CHANJO YA MDONDO WA KUKU

CHANJO YA MDONDO WA KUKU (KIDERI) – TEMEVAC

 

Chanjo yenye virusi hai vya mdondo vya I-2 inayohimili joto vinavyo kinga kuku dhidi ya ugonjwa wa mdondo. Mdondo ni ugonjwa wa kuambukiza kwenye kuku na jamii zingine za ndege unaosababishwa na virus aina ya para-myxovirus. Ndege wanopata ugonjwa huu ni kuku, batamzinga, bukini, bata, kanga, kware and ndege wengine wasiofugwa na waliohifadhiwa. Dalili zake ni pamoja na kuharisha kinyesi cha kijani, mafua makali, kizunguzungu na hatimaye kifo. TEMEVAC inazalishwa kulingana na viwango vya ubora chini ya muongoza wa viwango vya ubora wa ISO 9001:2015 pamoja na viwango na miongozo ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).

 

Mnyama mlengwa na namna ya kuchanja

 

Chanjo hii itolewe kwa ndege ambaye haonyeshi dalili zozote za kuumwa. Chanjo hii itumike moja kwa moja toka kwenye chupa ya chanjo na isichanganywe na kitu chochote. Weka tone moja la chanjo kwenye jicho moja kwa kila kuku. (Ndege wengine wanaweza kuchanjwa na TEMEVAC kama bata, kanga, bata mzinga). Msaidizi abebe kuku anayetakiwa kuchanjwa kiupande huku jicho moja likiwa limeelekezwa kwa mchanjaji. Mchanjaji ashike kichwa cha kuku na afungue jicho kwa kutumia dole gumba na kidole kinachofuata dole gumba vyote vya mkono mmoja. Mchanjaji ashika chupa ya chanjo kwenye mkono mwingine, ainamishe kuelekea kwenye jicho, abonyeze taratibu ili tone lidondoke kwenye jicho la kuku na ahakikishe chanjo inasambaa kwenye jicho zima kabla kuku hajaachiwa.

 

Uhifadhi na mwonekano

 

Chanjo ya TEMEVAC ni kimiminika kwenye chupa ya mililita 3 (dozi 50), mililita 5 (dozi 100) na mililita 10 (dozi 200). Huhifadhiwa katika chupa ya plastiki na ina mfuniko wenye sili. Chupa zina rangi ya buluu (dozi 50) na rangi nyeupe (dozi 100 na 200). Hifadhi ndani ya jokofu katika jotoridi la 2℃ – 8℃ kwa kipindi kisichozidi miezi minne toka tarehe ya kuzalishwa. Kamwe isiwekwe kwenye sehemu ya kugandisha barafu. Kama hakuna Jokofu, itunzwe sakafuni/kivulini kwenye hali ya ubaridi na itumiwe haraka iwezekanavyo. Chanjo itumike katika kipindi cha siku 7 baada ya kufunguliwa kama itakuwa inarudishwa kwenye jokofu baada ya kutumiwa.

 

Usafirishaji

 

Chanjo isafirishwe kwenye hali ya ubaridi ndani ya kasha la baridi (cool box) lenye barafu au chupa ya chai (thermos) yenye vipande vya barafu. Kama hakuna uwezekano wa kupata barafu, chupa yenye chanjo inaweza kuvilingishwa kwenye kitambaa cha pamba kilicholoweshwa maji ya baridi na kuwekwa kwenye mfuko wa kitambaa au kapu lenye matundu wakati wa kusafirishwa na itumike haraka.

 

Mambo ya kuzingatia

 

  • Epuka kuweka chanjo kwenye mwanga wa jua;
  • Chanja kuku mwenye afya njema tu;
  • Kuku ni salama kuliwa hata baada ya kuchanjwa;
  • Chanjo hii haina madhara kwa vifaranga, ukuaji au utagaji wa mayai;
  • Kuku anaweza kupewa chanjo ya TEMEVAC kuanzia umri wa wiki 1-2 na
  • Kuku wachanjwe kila baada ya miezi 4.

 

Kwa msaada zaidi wa kitalaam wasiliana na tabibu wa wanyama alie karibu nawe.

 

TEMEVAC inazalishwa na:

TAASISI YA CHANJO TANZANIA (TVI),

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania,

S.L.P. 30137,

Kitalu Na. 34, Pangani area, Kibaha.

Simu: 0733 282 032/0785 553 260

Baruapepe: tvi@tvla.go.tz

Kibaha – TANZANIA.