CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA KIMETA NA CHAMBAVU KWA NG’OMBE, MBUZI NA KONDOO

CHANJO YA TECOBLAX

 

TECOBLAX ni chanjo inayokinga ng’ombe, kondoo na mbuzi dhidi ya ugonjwa wa Kimeta na Chambavu. Chambavu ni ugonjwa unaoathiri ng’ombe na kondoo na hupelekea kifo. Ugonjwa wa chambavu husababishwa na kimelea cha Clostridium chauvoei. Kimeta ni ugonjwa unasababiashwa na kimelea cha Bacillus anthracis. TECOBLAX inazalishwa kulingana na vijwango vya ubora chini ya muongoza wa viwango vya ubora wa ISO 9001:2015 pamoja na viwango na miongozo ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).

 

Mnyama mlengewa na jinsi ya kutumia

 

Chanjo ya TECOBLAX inatolewa kwa ng’ombe, kondoo na mbuzi wa kuanzia umri wa miezi 6 na kuendelea. Tikisa vizuri chupa ya chanjo kabla ya kuvuta chanjo. Ondoa sili ya kifuniko cha bati. Tumia bomba la sindano lililo safi, vuta mililita 2 za chanjo (dozi moja kwa ng’ombe) au mililita 1 (dozi moja kwa kondoo au mbuzi) kutoka kwenye chupa. Sindano iliyotumika kuvuta dawa iache palepale kwenye chupa ili kuepuka kuchafua chanjo. Tumia sindano safi kwenye bomba lenye chanjo na choma chanjo chini ya ngozi nyuma ya bega au kwenye ngozi iliyoninginia maeneo ya shingo kwenye mnyama aliyedhibitiwa kikamilifu. Rudia chanjo kila baada ya miezi 12.

 

Uhifadhi na muonekano

 

Chanjo ya TECOBLAX huhifadhiwa katika chupa ya kioo ya rangi ya kahawia yenye ujazo wa mililita 100 yenye kizibo cha plastiki na kifuniko cha bati chenye sili. Chanjo ni kimiminika chenye rangi ya kijivujivu na weupe uliofifia. Chanjo ya TECOBLAX itunzwe/ihifadhiwe kwenye jokofu lenye jotoridi la 2℃-8℃. Isiwekwe kwenye sehemu ya jokofu inayogandisha. Chanjo iliyobaki yaweza kutumika ndani ya siku 7 ikiwa itahifadhiwa kwenye jokofu la jotoridi 2-8℃.

 

Usafirishaji

 

Chanjo isafirishwe katika mnyororo wa ubaridi; iwekwe ndani ya kasha la kutunza ubaridi lenye barafu (2℃-8℃) mpaka wakati wa kumchoma mnyama.

 

Mambo ya kuzingatia

 

  • Uchanjaji wa TECOBLAX ufanywe na Daktari wa wanyama au Daktari msaidizi waliosajiliwa na baraza la veterinary Tanzania (VCT);
  • Usichanje wanyama wagonjwa;
  • Wanyama wachanjwe kila baada ya miezi 12;
  • Usitumie chanjo kama sili imeharibika;
  • Chanja wanyama wenye umri wa miezi sita (6) au zaidi na
  • Chupa zilizoisha chanjo, sindano, gloves na vifaa vyote vilivyotumika vichomwe kwa moto mkali au visafishe na kipukusi kabla ya kuvitupa au kuvichoma.

 

Kwa msaada zaidi wa kitalaam wasiliana na tabibu wa mifugo alie karibu nawe.

 

Chanjo ya TECOBLAX inazalishwa na:

TAASISI YA CHANJO TANZANIA (TVI),

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).

S.L.P. 30137,

Kitalu Na. 34, Pangani area, Kibaha.

Simu: 0733 282 032/0785 553 260

Baruapepe: tvi@tvla.go.tz

Kibaha – TANZANIA.