CHANJO DHIDI YA HOMA YA MAPAFU YA MBUZI (CPPP)
CHANJO YA CAPRIVAC
CAPRIVAC ni chanjo iliyotengenezwa kwa vimelea vilivyouwawa inayotumika kuchanja mbuzi dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu. Ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya Mbuzi ni ugonjwa hatari wa mbuzi unaosababishwa na vimelea vya Mycoplasma capricolum subspecies capripneumoniae (Mccp). CAPRIVAC inazalishwa kulingana na vijwango vya ubora chini ya muongoza wa viwango vya ubora wa ISO 9001:2015 pamoja na viwango na miongozo ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).
Mnyama mlengwa na jinsi ya kutumia
Chanjo ya CAPRIVAC inatolewa kwa mbuzi ambaye hana dalili zozote za ugonjwa mwenye umri wa miezi mitatu (3) au zaidi na asiye na mimba. Tikisa chanjo kabla ya kumchoma mnyama. Binua sili, vuta chanjo mililita 1 (dozi moja) ya chanjo kutoka kwenye chupa kwa kutumia bomba safi la sindano. Choma chanjo chini ya ngozi iliyo nyuma ya bega. Ili kuepuka kuchafua chanjo, sindano iliyotumika kuvuta dawa iache palepale kwenye chupa, chomoa bomba pekee. Chanjo iliyofunguliwa itumike ndani ya saa tatu (3). Chanjo irudiwe baada ya miezi 12.
Uhifadhi na mwonekano
Chanjo ya CAPRIVAC huhifadhiwa katika chupa ya kahawia ya kioo yenye kifuniko cha plastiki na cha bati chenye sili. CAPRIVAC ipo katika hali ya kimiminika na huhifadhiwa katika chupa yenye ujazo wa mililita 50 (dozi 50). Ihifadhiwe kwenye ubaridi wa 2℃– 8℃. Isiwekwe kwenye sehemu ya kugandisha barafu.
Usafirishaji
Chanjo ya CAPRIVAC isafirishwe katika mnyororo wa ubaridi; iwekwe ndani ya kasha la baridi lenye barafu (2℃ - 8℃) mpaka wakati wa kumchoma mnyama.
Mambo ya kuzingatia
- Uchanjaji wa CAPRIVAC ufanywe na Daktari wa wanyama au Daktari msaidizi waliosajiliwa na baraza la veterinary Tanzania (VCT);
- Usichanje mbuzi wagonjwa au wenye mimba;
- Mbuzi achanjwe CAPRIVAC kila baada ya miezi 12;
- Chupa ikishafunguliwa itumike ndani ya saa tatu;
- Chanjo hii huchanjwa Mbuzi mwenye umri wa miezi mitatu na kuendelea na
- Usitumie chanjo kama sili imeharibika.
Kwa msaada zaidi wa kitalaam wasiliana na tabibu wa mifugo alie karibu nawe.
CAPRIVAC inazalishwa na:
TAASISI YA CHANJO TANZANIA (TVI),
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).
S.L.P. 30137,
Kitalu Na. 34, Pangani area, Kibaha.
Simu: 0733 282 032/0785 553 260
Baruapepe: tvi@tvla.go.tz
Kibaha – TANZANIA.