CHANJO DHIDI YA UGONJWA WA CHAMBAVU KWA NG’OMBE, MBUZI NA KONDOO

CHANJO YA CHAMBAVU

 

Chanjo ya Chanbavu ni chanjo inayozalishwa kwa vimelea vilivyouawa inayokinga ng’ombe na kondoo dhidi ya ugonjwa wa Chambavu. Chambavu ni ungonjwa unaosababisha vifo kwenye ng’ombe na kondoo unaosababishwa na kimelea aitwaye Clostridium chauvoei. Chanjo ya Chambavu inazalishwa ikiwa ni sumu ya kimelea cha Clostridium Chauvoei (Clostridium Chauvoeicytotoxin A - CctA proteins) toka kwenye kimelea kilichouawa kwa fomalini. Chanjo ya Chambavu inazalishwa kulingana na viwango vya ubora chini ya muongozo wa viwango vya ubora wa ISO 9001:2015 pamoja na viwango na miongozo ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).

 

Mnyama mlengwa na jinsi ya kutumia

 

Chanjo ya Chambavu ni kwa ajili ya kuchanja ng’ombe na kondoo ambao hawana ugonjwa dhidi ya ugonjwa wa Chambavu. Wakati wa kuchanja tumia bomba na sindano salama na tikisa chupa ya chanjo kabla ya kuvuta chanjo toka kwenye chupa. Epuka kuchafua kifuniko cha chanjo iliyo kwenye matumizi; kwa kuacha sindano iliyotumika kuchukua chanjo kwenye chupa kwa ajili ya kutumika wakati wa kuchukua chanjo tena. Choma mililita mbili (2ml) za chanjo chini ya ngozi nyuma ya bega au kwenye ngozi maeneo ya shingo kwenye mnyama aliyedhibitiwa kikamilifu. Chanja wanyama wenye umri wa miezi sita (6) na kuendelea kila baada ya miezi 12.

 

Uhifadhi na mwonekano

 

Chanjo ya Chambavu iko kwenye kimiminika cha rangi ya kijivu iliyopauka kwenye chupa ya kioo ya kahawia ya ujazo wa mililita 100 sawa na dozi 50. Chanjo itunzwe katika ubaridi wa 2℃ – 8℃. Isiweke kwenye eneo la kugandish barafu. Ikitunzwa kwa ubaridi wa 2℃ - 8℃ inaweza kubaki na ubora wake kwa miezi 12.

 

Usafirishaji

 

Chanjo ya chambavu inabidi isafirishwe kwenye mnyororo wa baridi (2℃ – 8℃) kwa kutumia kasha la kutunza ubaridi lenye barafu mpaka wakati wa kutumiwa.

 

Mambo ya kuzingatia

 

  • Uchanjaji dhidi ya Chambavu ufanywe na Daktari wa wanyama au Daktari msaidizi waliosajiliwa na baraza la veterinary Tanzania (VCT);
  • Usichanje wanyama wagonjwa;
  • Wanyama wachanjwe kila baada ya miezi 12;
  • Usitumie chanjo kama sili imeharibika;
  • Chanja wanyama wenye umri wa miezi sita (6) au zaidi na
  • Chupa zilizoisha chanjo, sindano, gloves na vifaa vyote vilivyotumika vichomwe kwa moto mkali au visafishe na kipukusi kabla ya kuvitupa au kuvichoma.

 

Kwa msaada zaidi wa kitalaam wasiliana na tabibu wa mifugo alie karibu nawe.

 

Chanjo ya Chambavu inazalishwa na:

TAASISI YA CHANJO TANZANIA (TVI),

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA).

S.L.P. 30137,

Kitalu Na. 34, Pangani area, Kibaha.

Simu: 0733 282 032/0785 553 260

Baruapepe: tvi@tvla.go.tz

Kibaha – TANZANIA.