Wafugaji Wanufaika na Huduma za TVLA Katika Maonyesho ya Sabasaba

Na Daudi Nyingo
Wafugaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wameendelea kunufaika na huduma za kitaalamu zinazotolewa na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
TVLA, ambayo ni taasisi chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imeshiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu, ushauri na huduma muhimu zinazohusu afya ya mifugo, udhibiti wa magonjwa, pamoja na kuhamasisha matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa hapa nchini.
Katika banda lake, wakala imeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wafugaji na wadau wa sekta ya mifugo, zikiwemo elimu kuhusu umuhimu wa chanjo bora kama TEMEVAC kwa kuku (mdondo), BOVIVAC kwa ng’ombe (homa ya mapafu), na CAPRIVAC kwa mbuzi.
Huduma nyingine ni uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia za kisasa kama ELISA, PCR na hadubini, pamoja na ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu na dawa za mifugo, kufanya uchunguzi wa ubora wa vyakula vya mifugo kwa lengo la kuhakikisha lishe bora na afya ya mifugo inaimarika.
Akizungumza Julai 12, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu ushiriki wa TVLA kwenye maonesho hayo, Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, alisema kuwa ushiriki wa Wakala kwenye maonesho ni sehemu ya mkakati wa Serikali kufikisha huduma bora za kitaalamu karibu zaidi na wafugaji.
“Kupitia Sabasaba, tunawafikia maelfu ya wafugaji moja kwa moja. Tunawahimiza wachukue sampuli za mifugo yao pale wanapohisi dalili za magonjwa na kuzifikisha kwenye maabara zetu kwa uchunguzi wa kitaalamu kabla ya matibabu,” alisema Dkt. Bitanyi.
Wafugaji waliotembelea banda la TVLA wamepongeza huduma zinazotolewa, wakisema zimewasaidia kupata uelewa sahihi wa namna ya kuboresha ufugaji wao kwa njia salama na za kisasa.
“Kwa mara ya kwanza nimepata elimu sahihi kuhusu sababu zinazoweza kufanya chanjo kutofanya kazi. Nimeelewa kuwa chanjo inapaswa kutolewa kwa mnyama ambaye hana ugonjwa wowote, hivyo ni muhimu sana kupima mifugo kabla ya kuwachanja ili kuhakikisha chanjo inafanya kazi kwa ufanisi,” alisema Bw. Ramadhani Shabani, mfugaji kutoka Kisarawe.
Kupitia ushiriki katika Sabasaba, TVLA inalenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu afya ya mifugo, usalama wa chakula, na umuhimu wa kuchukua hatua mapema ili kuzuia milipuko ya magonjwa hatari.
Aidha, Wakala inaendelea kuhamasisha wafugaji kushirikiana na maabara za Serikali kwa ajili ya uchukuaji na uchambuzi wa sampuli, ili kuhakikisha matibabu yanafanyika kwa usahihi na kwa ufanisi zaidi.
MWISHO