TVLA Yapongezwa kwa Kuimarisha Afya za Mifugo Nchini

Na Daudi Nyingo
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate S. Semesi, ameipongeza Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa huduma bora inazozitoa, hasa katika uchunguzi wa magonjwa ya wanyama na uzalishaji wa chanjo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya ya mifugo nchini.
Dkt. Semesi alitoa pongezi hizo Julai 13, 2025 alipofanya ziara katika banda la TVLA lililopo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
“TVLA imeendelea kuwa mhimili muhimu katika utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya Chanjo kwa Mifugo iliyozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa ziara yake mkoani Simiyu. Mafanikio ya taasisi hii yanaonekana moja kwa moja katika kupungua kwa milipuko ya magonjwa ya mifugo,” alisema Dkt. Semesi.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho wa uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi na teknolojia inayotumika katika maabara za TVLA, huku akisisitiza umuhimu wa kuendeleza tafiti za kina kuhusu magonjwa ya mifugo ili kulinda afya za mifugo nchini.
Katika banda la TVLA, wafugaji mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi wameendelea kupata elimu kuhusu afya ya mifugo, matumizi sahihi ya chanjo, namna ya kutambua magonjwa, pamoja na ushauri juu ya ubora wa vyakula vya mifugo.
MWISHO