TVLA YAKUSANYA SAMPULI ZA NGURUWE WALIOSHAMBULIWA NA UGONJWA PWANI
TVLA YAKUSANYA SAMPULI ZA NGURUWE WALIOSHAMBULIWA NA UGONJWA PWANI

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kupitia Kituo chake cha Magonjwa Ambukizi na Bayoteknolojia (CIDB), imechukua sampuli za nguruwe waliodhaniwa kushambuliwa na ugonjwa hatari katika kijiji cha Saga, mkoani Pwani, kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.

Zoezi hilo limefanyika Julai 23, 2025, katika shamba la Dkt. Dismas Raphael, ambapo nguruwe kadhaa walionyesha dalili za ugonjwa unaodhaniwa wa Homa ya Nguruwe (African Swine Fever – ASF), ambayo ni miongoni mwa magonjwa hatari yanayoshambulia mifugo hiyo na kusababisha vifo vya ghafla.

Meneja wa Kituo cha CIDB, Dkt. Mathias Mkama, alisema kuwa dalili zilizoripotiwa zinaashiria uwezekano mkubwa wa ASF, ambayo husababishwa na virusi vinavyoenezwa hasa na kupe kwa njia ya kunyonya damu kutoka kwa mnyama aliyeathirika kisha kumwambukiza mwingine.

“Mbali na kupe, maambukizi ya ASF yanaweza kusambazwa kupitia mabaki ya chakula chenye vimelea, vifaa vya huduma vinavyotumika kwa nguruwe zaidi ya mmoja bila kutakaswa, pumba, na hata sindano zinazotumika kwa pamoja bila kuchukuliwa tahadhari,” alisema Dkt. Mkama.

Naye Daktari wa Mifugo kutoka kituo cha CIDB, Dkt. Jumanne Jumbe, ametoa ushauri kwa wafugaji wote kuacha kuwalisha nguruwe wao mabaki ya chakula chenye nyama au mifupa ya nguruwe kutoka vyanzo visivyo salama. Alisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuchangia kuingiza virusi vya ASF shambani na kuongeza hatari ya maambukizi kwa kasi.

“Ni muhimu wafugaji kuweka utaratibu wa kudhibiti uingiaji wa watu kwenye mabanda ya nguruwe, na wataalamu wa mifugo wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa wasije wakawa chanzo cha kueneza vimelea kutoka shamba moja kwenda jingine,” alieleza Dkt. Jumbe.

Kwa upande wake, Dkt. Dkt. Dismas Raphael ambaye ndiye mmiliki wa shamba lililoathirika, alisema kuwa, alianza kubaini dalili zisizo za kawaida kwa watoto wa nguruwe wake, ikiwa ni pamoja na kuacha kula, kutoa mapovu mdomoni na hatimaye kufa, hali iliyodumu kwa wiki mbili na kusababisha vifo vya watoto wa nguruwe 11 kati ya 15 waliokuwepo.

Aliongeza kuwa alijalibu kutumia dawa za kupunguza maumivu kwa ushauri wa bwana mifugo lakini hali iliendelea kuwa mbaya na baadae aliamua kuwasiliana na ofisi ya TVLA.

Wataalamu kutoka TVLA wameahidi kukamilisha uchunguzi wa sampuli hizo haraka iwezekanavyo ili kutoa taarifa rasmi ya kitu kinachowasumbua Nguruwe hao na mapendekezo ya kudhibiti milipuko ya magonjwa ya wanyama.