TVLA Yadumisha Afya na Mshikamano Kupitia Michezo ya Ndani
TVLA Yadumisha Afya na Mshikamano Kupitia Michezo ya Ndani

Na Daudi Nyingo

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, leo Julai 18, 2025 amekuwa mgeni rasmi katika mechi ya kirafiki ya mpira wa miguu iliyowakutanisha watumishi kutoka idara mbalimbali zilizo chini yake.

Mchezo huo uliopigwa saa 10 jioni katika uwanja wa Mifugo Complex Arena, Veterinari – Temeke, uliwashindanisha Muunganiko wa TVI na CIDB dhidi ya Muunganiko wa TVLA Makao Makuu na CVL, ambapo timu ya TVLA-HQ/CVL iliibuka kidedea kwa ushindi wa magoli 4-2.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Dkt. Bitanyi aliwapongeza wachezaji wote kwa ushiriki wao na kuonesha mshikamano kupitia michezo, huku akisema kuwa michezo ni sehemu muhimu ya afya ya mwili na akili, hasa katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

"Moja ya majukumu ya TVLA ni kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza, na kwa kuwa michezo ni njia muhimu ya kuzuia magonjwa hayo, nawahakikishia kuwa nitayapa kipaumbele masuala ya michezo katika mwaka huu wa fedha.”

“TVLA sasa ina timu nzuri ya michezo. Tumejipanga kushiriki kikamilifu mashindano ya SHIMIWI na SHIMUTA mwaka huu. Nitahakikisha michezo inapewa kipaumbele ndani ya mwaka huu wa fedha"alisema Dkt. Bitanyi.

Katika kuthamini jitihada za wachezaji, Dkt. Bitanyi alitoa zawadi ya Shilingi milioni mbili kwa timu iliyoshinda na shilingi laki nane kwa timu iliyopoteza mchezo, kama motisha na kuhamasisha ushiriki zaidi wa michezo kazini.

Kwa mujibu wa waandaaji, mchezo wa marudiano unatarajiwa kuchezwa Ijumaa ya Julai 25, 2025, katika uwanja wa Kibaha, mkoani Pwani, kuanzia saa 10 jioni.

Mwisho