TVLA YATOA MSAADA WA FIMBO 20 ZA KUTEMBELEA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA MACHO
TVLA YATOA MSAADA WA FIMBO 20 ZA KUTEMBELEA KWA WATU WENYE ULEMAVU WA MACHO

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imekabidhi msaada wa fimbo 20 zenye thamani ya tsh. 1,000,000/= kwa watu wenye ulemavu wa macho (wasioona) kwa Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam ambazo zitawasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 17,2022 Jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano hayo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi amesema kuwa wamekabidhi Fimbo hizo kama shukrani kwa mwenyezi Mungu kwa yale ambayo wametendewa na pia kuguswa na hali ambayo wanapitia walemavu hao.

"Tumerudi kwao kuonesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, kwasababu hali ambayo wanapitia hawakuitaka wao ni majaaliwa ya Mwenyezi Mungu ambayo inaweza kumtokea mtu yeyote ambaye anaona leo". Amesema Dkt. Bitanyi

Aidha Dkt. Bitanyi amesema TVLA wamekuwa wakishashirikiana na makundi mbalimbali ya walemavu ikiwa kama uwajibikaji kwa kuwasidia watu wenye mahitaji kwenye jamii mfano kikundi cha Magomeni wameshapatiwa msaada kuchangia kupatikana kwa viti mwendo ambavyo Chama kili kilikuwa kinafanya kukusanya kwa ajili ya wanachama wake.

Nae Katibu wa Chama cha TLB, Bw. Protase Mutakyanga ameipongeza TVLA kwa msaada ambao wamewapatia kwani fimbo hizo ni ghali kwa mwananchi mmoja mmoja kwa wasioona ambapo imekuwa ni changamoto kwa upande wao kuzipata.

Hata hivyo Bw.Mutakyanga amewaomba TVLA kuendelea kufanya tafiti na kuzalisha na chochote kitachopatikana waendelee kutoa kwa watu wenye mahitaji maalumu ili kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo.

Aliongeza kuwa walipeleka ombi lao mnamo Mei 24, 2022 na Mtendaji Mkuu wa TVLA aliwajibu barua yao kwamba Wakala wapo tayari kuwasaidia takribani fimbo 20 kwa ajili ya wanachama wa chama hicho.

"Chama cha Wasiiona Wilaya ya Temeke kina jumla ya wanachama 223 ambapo wote ni wenye ulemavu wa macho ambao wanahitaji fimbo, tunashukuru kwa msaada huu kwasababu umekuja katika wakati muhimu sana kwani ni siku ya kesho tu tutaanza safari ya kuelekea mkoani Manyara kwa ajili ya maadhimisho ya kimataifa ya Fimbo nyeupe". Amesema