SERIKALI YAWAPIGA MSASA WAZALISHAJI, WAUZAJI VYAKULA VYA MIFUGO
SERIKALI YAWAPIGA MSASA WAZALISHAJI, WAUZAJI VYAKULA VYA MIFUGO

Na Daudi Nyingo
Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Taasisi yake ya Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) imewapa mafunzo ya siku moja wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo kutoka mikoa ya Pwani na Dar-es-salaam yaliyofanyika Disemba 20, 2023 kwenye ofisi za Taasisi hiyo Temeke jijini Dar-es-salaam.


Akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Stella Bitanyi amesema kuwa hatua hiyo imetokana na malalamiko ambayo Serikali imekuwa ikiyapokea hasa kutoka kwa wafugaji wa kuku ambao wamekuwa wakilalamikia udumavu wa kuku unaohusishwa na ubora hafifu wa vyakula vya mifugo vilivyopo sokoni.


“Tumeona tuwaite na kuwapa mafunzo haya kwa sababu hatutaki kurudi kwenye kile kipindi ambacho wafugaji walikuwa wanaagiza vyakula vya mifugo kutoka nje ya nchi kwa sababu kufanya hivyo ni kuua viwanda vyetu vya ndani” Ameongeza Dkt. Bitanyi.


Aidha Dkt. Bitanyi amesisitiza kuwa Taasisi yake itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya mifugo ikiwa ni pamoja na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kukagua utekelezaji wa yale waliyoelekezana kwenye mafunzo hayo kazi itakayofanywa na kikosi kazi kutoka kwenye Taasisi hiyo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara yake ya Nyanda za malisho na vyakula vya Mifugo na wakaguzi wa vyakula vya Mifugo kutoka kwenye Mikoa na Wilaya zote nchini.


Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za vyakula vya Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Rodgers Shengoto amesema kuwa Wizara yake imetumia mafunzo hayo kuwasisitiza wadau wote waliopo kwenye tasnia ya vyakula vya Mifugo kuhakikisha wanasajili shughuli zao kwa mujibu wa sheria ya Maeneo ya Malisho sura namba 180 pamoja na kanuni zake.


“Lakini pia msitumie nafaka au rasilimali za vyakula zisizofaa kwa matumizi ya binadamu kutengenezea vyakula vya Mifugo kwa sababu mnyama akiathirika humuathiri pia mlaji anayekula nyama ile” Ameongeza Bw. Shengoto.


Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni mzalishaji wa vyakula vya Mifugo Bw. Mohammed Mshana ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha mafunzo hayo ambapo ameshauri zoezi hilo liwe endelevu ili waweze kuendelea kutekeleza shughuli zao kwa tija.


Akielezea namna mafunzo hayo yalivyomuwezesha kufahamu matumizi sahihi ya chanjo za mifugo, mmoja wa washiriki ambaye ni mfugaji kutoka Wilaya ya Kigamboni Bi. Albina John amesema kuwa sasa anatarajia kuanza kutibu mifugo yake kwa wakati tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo chanjo alizokuwa akinunua kutoka nje ya nchi zilikuwa hazimfikii kwa wakati.


Mafunzo hayo yamefanyika ikiwa ni wiki chache tangu kufanyika kwa operesheni maalum ya ukaguzi wa viwanda na maduka yanayouza vyakula vya Mifugo ambayo iliendeshwa na Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) na kubaini dosari mbalimbali kwa wadau hao wa ufugaji nchini