RC Dodoma aitaka TVLA kuongeza kasi utoaji huduma kwa Wafugaji

Na Daudi Nyingo
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameitaka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuongeza kasi ya uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wafugaji hasa katika eneo la uchanjaji wa Mifugo Vijijini.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo tarehe 03 Agosti, 2024 alipotembelea Banda la TVLA lililopo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea kufanyika katika uwanja wa Nzuguni jijini Dodoma.
“Serikali mwaka huu imetenga bajeti kubwa kwa ajili ya kutoa Chanjo za Mifugo bure kwa wafugaji, hakikisheni mnashirikiana na Halmashauri kuwafikia wafugaji wote kote nchini kuchanja mifugo yao na muwapatie elimu sahihi ya matumizi ya chanjo. Vilevile naishauri TVLA kuangalie namna ya kuwa na ofisi hadi ngazi ya Wilaya na kata ili kusogeza huduma karibu na wafugaji.” Alisema Mhe. Senyamule
Daktari wa Mifugo Mtafiti wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Isaac Mengele Alisema kuwa TVLA inashiriki Maonesho ya Nanenane kwa lengo la kutoa elimu ya huduma bora za Maabara za Veterinari, kutoa elimu ya utafiti juu ya magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa hayo pamoja na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya Chanjo za Mifugo kwa wafugaji na wadau wanaotembelea banda la TVLA.
“TVLA imejipanga kuimarisha uzalishaji endelevu katika sekta ya Mifugo, Usalama wa Chakula na kuchangia kwenye Uchumi wa Taifa kupitia utoaji wa huduma bora zenye gharama nafuu za uchunguzi na utambuzi, uzalishaji wa bidhaa za veterinari na kufanya tafiti za magonjwa ya Mifugo na wadudu waenezao magonjwa hayo.” Alisema Dkt Mengele.
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) inatoa huduma za uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya Mifugo, Uzalishaji na Usambazaji wa Chanjo za Mifugo, Uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, Usajili na uhakiki wa ubora wa Viuatilifu vya Mifugo, utafiti wa magonjwa ya Wanyama pamoja na huduma ya ushauri na Mafunzo.
MWISHO