Prof. Shemdoe asisitiza Matumizi sahihi ya Chanjo za Mifugo Kuinua soko la nyama nje ya nchi
Prof. Shemdoe asisitiza Matumizi sahihi ya Chanjo za Mifugo Kuinua soko la nyama nje ya nchi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewataka Wafugaji kote Nchini kuacha kufuga kwa mazoea na kuzingatia matumizi sahihi ya chanjo za mifugo zinazozalishwa na Serikali ili kujihakikishia usalama wa mifugo yao na kujipatia kipato kwa kuuza nyama zenye ubora kwenye masoko ya kimataifa.

 

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Mei 12, 2023 alipofanya ziara ya kutembelea Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa lengo la kufahamu kazi zinazofanywa na Wakala na kujionea shughuli mbalimbali za kimaabara.

 

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa fedha ambazo amekuwa akizitoa hapa kuongeza vifaa na kuzifanya maabara zetu ziwe za kisasa zaidi, mimi kama Mtendaji Mkuu wa Wizara niahidi kuendelea kuiangalia Wakala hii kwa jicho tofauti, kwani ni eneo ambalo tukiimarika zaidi hata mifugo yetu itaimarika na mifugo ikiimarika tutapata masoko mengi ya nje ya Nchi.” Alisema Prof. Shemdoe.

 

Akiwa katika ziara hiyo Katibu Mkuu alisema kwamba kazi kubwa inayofanywa na Wakala inasaidia nchi kutambua magonjwa ya Mifugo ambayo yapo nchini ili kuweza kuyazuia au kuyaondoa kabisa kwani ni kazi ambayo inasaidia kuiweka mifugo isiambukizwe au kupata magonjwa mbalimbali.

 

Sambamba na hilo aliongeza kuwa kwa miaka michache iliyopita Tanzania ilikuwa inapeleka nyama nje ya nchi tani elfu moja lakini mwaka huu wa fedha unaoisha tumeshavuka tani elfu 12, na kitendo cha Wakala kupata Ithibati mbalimbali itatusaidia kupata masoko ya Nyama mengi zaidi ndani na nje ya nchi.

 

“Nimependezwa na namna mlivyojitahidi kupata Ithibati ya vipimo muhimu 10 kwa ajili ya kuhudumia wanyama wetu mbalimbali ndani ya nchi, vilevile nimependezwa na kazi inayoendelea ya uzalishaji wa Chanjo ambapo mnazo chanjo za aina saba (7) zinazoendelea kutumika sambamba na hayo nimefurahishwa na jitahada zenu za kuendelea kutafuta Ithibati za Chanjo hizo ili zianze kutumika kimataifa, vilevile nimefurahishwa na miradi yenu ya kiutafiti iliyopo.” Alisema Prof. Shemdoe.

 

 

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe kwa kutenga muda wake kutembelea Wakala, kufahamu kazi zinazofanywa na kujionea shughuli mbalimbali za kimaabara.

 

“Tunategemea ziara hii itazaa matunda kwani amejionea uwezo wa Wakala katika kuchunguza na kutambua magojwa ya mifugo nchini, katika uzalishaji wa Chanjo na utambuzi wa ubora wake, amejionea shughuli za usajili na udhibiti wa ubora wa viatilifu vya mifugo, amejionea uwezo kwenye tafiti pamoja na uboreshaji wa vyakula vya mifugo nchini." Alisema Dkt. Bitanyi.

 

Akiwasilisha taarifa yake Dkt. Bitanyi alisema kuwa jukumu la kuzalisha chanjo lilianza mwaka 2012 kwa kuanza kuzalisha chanjo moja dhidi ya ugonjwa wa Kideri au Mdondo kwa Kuku na kwa kipindi cha miaka sita kuanzia 2016/2017 hadi 2021/2022 Wakala imezalisha jumla ya dozi 325,979,034 za Chanjo za Mifugo.

 

Dtk. Bitanyi alisema kwamba watafanya kazi kwa weledi ili kutoa huduma bora na kuongeza tija na kuipeperusha vyema bendera ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini.

 

Katika ziara hiyo Katibu Mkuu aliweza kutembelea Maabara ya uhakiki usalama na ubora wa vyakula vya mifugo iliyoko katika Maabara Kuu ya Mifugo, Maabara ya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama na wadudu wanaoeneza magonjwa hayo (CVL), Maabara ya utambuzi wa magonjwa ya virusi ya mlipuko (CIDB), kiwanda cha kuzalisha chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo (TVI Kibaha).

 

MWISHO