KATIBU MKUU AKABIDHI MAGARI 2 TVLA
KATIBU MKUU AKABIDHI MAGARI 2 TVLA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Tixon Nzunda leo Mei 19,2022 amekabidhi magari mawili kwa vituo vya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania kwenye mikoa ya Arusha na Tabora.

Magari hayo yamenunuliwa na Wakala ya Maabara yya Veteinari Tanzania (TVLA) kwa kutumia fedha za mapato ya ndani kama ilivyopangwa katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/20022.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya makabidhiano ya magari hayo katika Ofisi za TVLA Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Nzunda amevitaka vituo ambavyo vimekabidhiwa magari hayo waende wakayatumie kwa shughuli za TVLA kwaajili ya mafunzo kwa wafugaji na wadau wao wanaozalisha chakula cha mifugo ili waweze kuongeza tija na kuongeza mapato zaidi kwa taasisi.

“Tumieni magari haya kwaajili ya kutangaza shughuli za taasisi na shughuli za mifugo na kuwafikia wafugaji kwa ukaribu zaidi ili tuweze kutoa chanjo kwa wakati, chanjo zikiwa salama na kuwafikia wadau wengi zaidi lakini kuongeza wigo wa utoaji wa chanjo kwenye mifugo yetu”. Amesema Bw.Nzunda.

Amesema suala la chanjo kwa mifugo na suala la uogeshaji wa mifugo halitakuwa jambo la hiari ni jambo la lazima kwasababu ni lazima tulinde ustawi wa Wanyama na tulinde ustawi wa wananchi kwasababu mifugo ni chakula kwahiyo lazima iwe na afya bora ili iweze kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa katika mazao yatokanayo na mifugo kwa maana ya nyama na maziwa.

Aidha amevitaka vyama vya wafugaji na taasisi za wafugaji kuunda ushirika kwaajili ya kutafuta fedha ya chanjo lakini pia kuogesha mifugo ili Tanzania iwe mahali salama kuendelea kupata masoko makubwa zaidi ya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt.Stella Bitanyi amesema magari hayo mawili yamenunuliwa kwa thamani ya shilingi Milioni 207 fedha ambazo ni mapato ya ndani.

Ameeleza kuwa malengo ya ununuzi wa magari hayo ni kwenda kutekeleza shughuli za Wakala katika vituo hivyo ambazo ni pamoja na kuwezesha utoaji huduma kwa wafugaji, kuwafikia wafugaji kwaajili ya utoaji wa elimu na mafunzo, shughuli za vituo za kila siku pamoja na kuwezesha uhamasishaji na uuzaji wa bidhaa za Wakala.

“Changamoto waliokuwa wanaipitia ya kukosa usafiri wa uhakika kwa sasa itaenda kwisha na hivyo tunatarajia kuongezeka kwa ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya Wakala katika vituo vyao”. Amesema Dkt.Stella.

MWISHO