Nafurahishwa na Huduma Mnazotoa-Magoti
Nafurahishwa na Huduma Mnazotoa-Magoti

Na Daudi Nyingo

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti ameipongeza Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kuendelea kutoa huduma kwa wafugaji hasa katika suala la utoaji wa huduma za Chanjo pamoja na elimu ya ufugaji.

Mhe. Magoti ameyasema hayo leo Julai 11, 2024 alipotembelea banda la TVLA, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es salaam (sabasaba) kwa ajili ya kupata elimu kuhusiana na huduma zinazotolewa na TVLA.

Sanjali na hilo ameiomba TVLA kuendelea kutoa elimu kwa kutembelea wafugaji hasa katika Wilaya ya Kisarawe ambapo vikundi vya wafugaji vinaanzishwa ili kuwapatia elimu ya ufugaji na udhibiti wa magonjwa ya Mifugo.

“Hongereni sana kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya kwa kutoa elimu ya Mifugo hasa katika uzalishaji wa Chanjo za Mifugo na huduma za utambuzi wa magonjwa kwani mnasaidia kudhibiti magonjwa na kupunguza hasara kutokana na madhara ya magojwa.”

“Wilaya ya Kisarawe imekusudia kuanzisha vikundi vya wafugaji ili kuweza kuinua uchumi wa wananchi, lakini wafugaji wetu bado hawana elimu ya kutosha kuhusiana na ufugaji, nawaomba mje kutoa elimu kwa wafugaji wetu ili wafuge kwa faida.” Alisema Mhe. Magoti.

Kwa upande wake Daktari Mtafiti wa Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA) Dkt. Fredy Makoga amemueleza Mhe. Magoti kuwa kuchanja Mifugo ni njia yenye gharama nafuu kudhibiti magonjwa ya Mifugo.

Dkt. Makoga aliongeza kuwa ni muhimu kwa wafugaji kuepuka kutibu Mifugo yao kiholela badala yake watumie huduma za Maabara na ushauri unaotelewa na TVLA kutambua magonjwa ya Mifugo ili kuweza kufanya matibabu sahihi kupunguza hatari ya usugu wa vimelea dhidi ya dawa mbalimbali ambayo ni hatari kwa afya za Mifugo na Binadamu.

Dkt. Makoga amemuahidi Mhe. Magoti kulifikisha ombi lake kwenye uongozi ili liweze kufanyiwa kazi.

MWISHO