DED Mbarali apongeza Huduma zinazotolewa na TVLA Sabasaba

Na Daudi Nyingo
Aomba wataalam Wakatoe Elimu Mbarali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali iliyopo Mkoa wa Mbeya Bw. Missana Kwangura ameipongeza Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba hasa kuhusiana na uchunguzi wa magonjwa ya wanyama na uchanjaji wa Mifugo ili kuwakinga na magonja mbalimbali.
Bw. Kwangura aneyasema hayo leo Julai 09, 2024 alipotembelea banda la TVLA lililopo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es salaam (sabasaba) kwa ajili ya kupata elimu kuhusiana na huduma zinazotolewa na TVLA katika uchunguzi wa magonjwa ya wanyama, uzalishaji na usambazaji wa Chanjo za Mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na wadudu waenezao magonjwa hayo pamoja na uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo.
“Mbarali tuna Mifugo mingi kwa sasa, ipo zaidi ya laki 6, wafugaji wengi bado hawajafahamu kwa undani umuhimu wa kuchanja Mifugo yao, kuichunguza magonjwa na kuipeleka kwenye majosho, naomba wataalam wa TVLA waje wasaidiane na wataalam wangu kusaidia kutoa elimu ili wafugaji wasiendelee kupoteza Mifugo yao, Mbarali Mifugo ni hazina kubwa.” Alisema Bw. Kwangura.
Naye Afisa Utafiti Mifugo wa Wakala ya Maabara ya Veterinari (TVLA) Bw. Denis Nyakalinga amemuahidi Mkurugeni wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali kulifikisha ombi lake kwenye uongozi ili liweze kufanyiwa kazi, kwani TVLA ipo kwa lengo la kuhakikisha inalinda afya za Mifugo nchini.
MWISHO