Bodi ya Ushauri TVLA yapongeza mafanikio, yatoa wito wa weledi na mshikamano kwa watumishi
Bodi ya Ushauri TVLA yapongeza mafanikio, yatoa wito wa weledi na mshikamano kwa watumishi

Na Daudi Nyingo

Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imepongeza hatua kubwa za maendeleo na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Wakala, ikiwemo kupata ithibati ya vipimo 10 vya kimaabara vinavyotambulika kimataifa (ISO/IEC 17025:2017 ACCREDITED) pamoja na kuhimiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano na weledi miongoni mwa menejimenti na watumishi wote.

Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TVLA kwa niaba ya wajumbe wa Bodi, Prof. Amandus P. Muhairwa, tarehe 15 Agosti 2025, katika Makao Makuu ya TVLA wakati wa ziara ya Bodi hiyo kutembelea Maabara Kuu ya Veterinari (CVL) pamoja na Kituo cha Magonjwa Ambukizi na Bayoteknolojia (CIDB).

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Bodi walipata maelezo ya kina kuhusu majukumu ya Wakala katika kufanya uchunguzi na utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya mifugo, usajili na uthibiti wa ubora wa viuatilifu vya mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama pamoja na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kiteknolojia katika kudhibiti magonjwa hatarishi. Aidha, wajumbe wa Bodi walipata maelezo kuhusu hatua za uchukuaji wa sampuli za wanyama na vyakula vya mifugo, kuanzia namna zinavyokusanywa, kuchunguzwa hadi majibu yanavyotolewa.

Prof. Muhairwa alieleza kuwa TVLA imekuwa nguzo muhimu katika kulinda afya ya mifugo na usalama wa chakula nchini. Alisisitiza kuwa msingi mkuu wa kuanzishwa Wakala hii ni kutumia huduma za veterinari katika kulinda afya ya mifugo, hivyo menejimenti inapaswa kusimamia misingi hiyo ipasavyo huku ikihakikisha watumishi wachanga wanajengewa uwezo kupitia uzoefu wa watumishi waliobobea ili kuzuia upotevu wa ujuzi.

Aidha, alihimiza kuwepo kwa mpango wa muda mfupi na mrefu katika kuboresha miundombinu ya maabara ikiwemo vifaa na majengo ambayo yalijengwa katika miaka ya 1960. Pia alielekeza umuhimu wa kuendana na teknolojia mpya bila kuacha mbinu za awali katika kuthibitisha uwepo wa magonjwa ya mifugo.

Mwenyekiti huyo wa Bodi alisisitiza kuwa mwelekeo wa TVLA unapaswa kuendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliodhamiria kuimarisha sekta ya mifugo ili kuchangia zaidi katika pato la Taifa na ustawi wa jamii.

Katibu wa Bodi ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, aliishukuru Bodi kwa pongezi na ushauri walioutoa na kuahidi kuwa menejimenti ya Wakala itayafanyia kazi kikamilifu ili kuboresha utendaji kazi wake. Aidha, tayari Wakala imeanza kutekeleza mpango kazi wa kuboresha mazingira ya kazi na miundombinu yake ikiwemo ununuzi wa vifaa vya maabara, magari na ukarabati wa majengo katika vituo vyake vyote nchini.

Kabla ya kuanza ziara hiyo, wajumbe walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika kusimamia utendaji kazi wa TVLA, ambapo mwezeshaji kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Wilbert Ndugulile aliwapitisha katika miongozo mbalimbali itakayowawezesha kutekeleza ipasavyo majukumu yao kama Bodi ya Ushauri.

Ziara hiyo ilihitimishwa kwa wajumbe kujionea shughuli za kitaalamu na miundombinu ya kisasa inayotumiwa na TVLA katika maabara zake, hatua inayothibitisha dhamira ya wakala huo katika kulinda na kukuza tasnia ya mifugo nchini.

MWISHO